Home » » SIKU YA CHAKULA KUADHIMISHWA KIGOMA

SIKU YA CHAKULA KUADHIMISHWA KIGOMA



na Betty Kangonga
KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma, amesema Siku ya Chakula Duniani mwaka huu kitaifa itafanyika mkoani Kigoma katika kijiji cha Kalinzi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kaduma alisema Watanzania wataungana na wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuienzi siku hiyo iliyoanza jana na kufikia kilele Oktoba 16 mwaka huu kwa kutambua mchango na umuhimu wa chakula katika jamii.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ushirika katika kilimo: Ufunguo wa kulisha dunia” ambayo inalenga kuonyesha umuhimu na nafasi ya ushirika katika kuzalisha chakula kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya watu wote na kwingineko duniani.
Alisema sherehe hizo zitafunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, na kufungwa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Kaduma alisema sherehe hizo zinatilia maanani umuhimu wa chakula na nafasi yake kwa jamii kwa kuonyesha mafanikio na changamoto za upatikanaji wake kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.
Alisema maadhimisho hayo yataenda sambamba na maonesho ya wadau wa kilimo na chakula vikiwemo vikundi vya wajasiriamali, wakulima, wavuvi, wafugaji na sekta binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa