Home » » WASHITAKIWA WAFANYA FUJO MAHAKAMANI, NI BAADA YA KESI YAO YA MAUAJI KUCHELEWESHWA, HAKIMU AWANYUKA KIFUNGO CHA MIEZI 6 JELA KWA UKOROFI

WASHITAKIWA WAFANYA FUJO MAHAKAMANI, NI BAADA YA KESI YAO YA MAUAJI KUCHELEWESHWA, HAKIMU AWANYUKA KIFUNGO CHA MIEZI 6 JELA KWA UKOROFI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu.
Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa Kigoma imewahuku kifungo cha miezi sita mahabusu watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya mauaji kufuatia kitendo cha kufanya fujo mahakamani wakilalamika kesi yao kuchukuliwa muda mrefu bila kutolewa hukumu.
Mahabusu waliohukumiwa kifungo hicho na Hakimu mkazi mkoa kigoma Emanuel Mrangu ni Maneno Kichako, Majuto Dunia na Haruni Petro ambao inaelezwa kuwa waliongoza mgomo na kufanya fujo mahakamani hapo wakishinikiza mgomo wa mahabusu kugoma kuingia mahakamani.
Mrangu aliwahukumu kifungo hicho cha miezi sita jela watuhumiwa hao kwa kosa la kufanya fujo mahakamani na kusema kuwa kama walikuwa na madai yao kuhusu kucheleweshwa kwa mwenendo wa kesi zao walipaswa wapeleke malalamiko hayo kwa kufuata taratibu za kimahakama lakini si kufanya fujo mahakamani na hivyo kesi mbalimbali zilizokuwa zikiendeshwa kusimama kwa muda.
Awali mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa mara baada ya karandinga la polisi lilipowasili mahakamani hapo mahabusu hao waligoma kushuka na badala yake walianza kupiga kelele huku wakifunga mlango wa kutokea katika gari hilo ili kuzuia polisi kushindwa kuwashusha.
Hali hiyo iliwalazimu askari walioongozana na gari hilo kulipeleka gari hilo kituuo kikuu cha polisi mjini Kigoma na hapo walianza kupewa kipigo ili kuwafanya kulainika na kuruhusu ratiba ya siku kuendelea.
Aidha kwa mujibu wa mashuhuda hao walieleza kuwa katika sarakasi hizo mahabusu mmoja aliumia kwa kile kinachoelezwa kuwa kizidiwa na kipigo kutoka kwa askari polisi na hivyo kukimbizwa hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu.
Kamanda wa polisi mkoa kigoma alikiri kutokea kwa mgomo huo wa mahabu na kusema kuwa ni hali ya kawaida lakini tatizo hilo liliisha katika muda mfupi ambapo alikana kuumizwa kwa mahabusu huyo kwa kipigo cha polisi badala yake alisema kuwa mahabusu huyo alianguka kutoka kwenye gari na kuumia.
Aidha Hakimu mkazi mfawidhi  mkoa kigoma, Emanuel Mrangu alikiri kuwepo kwa vurugu hizo na kusema kuwa waliohusika na vurugu hizo walikuwa ni mahabusu watatu ambao wanakabiliwa na kesi ya mauaji ambao wanalalamika kesi yao kuchukua muda mrefu bila kwisha.
Hata hivyo alisema kuwa amewasiliana na uongozi wa magereza mkoa Kigoma kuona namna gani suala kama hilo linapatiwa ufumbuzi ikiwemo suala la mchakato wa kesi kuchukua muda mrefu huku akitoa angalizo la kuwataka maafisa magereza kuandika barua za maombi wa mwenenndo wa kesi kukumbusha kushughulikiwa kwa kesi ambazo zimechukua muda mrefu bila kumalizika.
Jopo la waandishi wa habari lilitembelea pia hospitali ya mkoa kigoma Maweni na kupata taarifa za mahabusu aliyelazwa hospitalini hapo aliyefahamika kwa jina la maneno Kichako ambapo viongozi waandamizi hospitalini hapo waliakataa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kuhusu kuwepo kwa mahabausu huyo hospitalini hapo.
Aidha waandishi walifanikiwa kupata uthibitisho kutoka kwa mtumishi mmoja wa hospitali hiyo alieleza kuwa mahabusu huyo kwa sasa yuko Wodi namba saba lakini hakuna mwandishi yeyote ambaye anaruhusiwa kuingia wodini humo kwa sasa.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa