Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
WATU watatu wameuwawa Mkoani Kigoma akiwemo Mwenyekiti na kaimu Mwenyekiti wa kitongoji cha Mvugwe, baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika mto Malagarasi.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Mkoani hapa Kamanda wa Polisi Freisser Kashai alisema chanzo cha vifo hivyo ni watu wasiofahamika waliokuwa na silaha mbalimbali kumvamia bw Kazimoto Kazola (47) Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mvugwe eneo la Santole na kupora vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 1.4.
Kamanda Kashai alisema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 7/2012 majira ya saa tatu usiku wakati wakiendelea na uporaji huo bw Kazola alikimbia ambapo majambazi hao waligundua kuwa bw Kazola aliweza kumtambua mmoja wa majambazi hao na hivyo kumuahidi mke wake kuwa ni lazima watamuuwa ili kupoteza ushahidi.
Kashai alisema kuwa mnamo Octoba 8/2012 wananchi walianza msako wa kuwasaka majambazi hao ambapo walipata taarifa kuwa majambazi hao walikuwa wamehifadhiwa katika nyumba ya mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa.
Aidha alisema kuwa baada ya majambazi hao kugundua kuwa wananchi wamezingira nyumba waliyopo waliamua kufyatua risasi wakiwa ndani ambapo zilimpiga kichwani Venance Mathias (38), mkazi wa kijiji cha Mvugwe na kufa papohapo na huku Wilson Joramu (38) alijeruhiwa mguu wa kushoto.
Alisema kuwa katika tukio hilohilo, mnamo Octoba 9/2012 majira ya saa nne asubuhi mwili wa Kazimoto Kazola Mwenyekiti wa Mvugwe uliokotwa ukiwa unaelea katika mto wa Malagalasi ukiwa umefungwa ndani ya gunia, taarifa ya uchunguzi wa daktari ulithibitisha kifo hicho kilitokana na kuvunjwa shingo na kusema kuwa hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment