Home » » JK mgeni rasmi kongamano Kigoma

JK mgeni rasmi kongamano Kigoma

RAIS Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la kuimarisha uchumi katika Mkoa wa Kigoma Ujiji. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu, Issa Machibya, alisema kongamano hilo litafanyika Oktoba 10 mwaka huu.

Alisema kuwa litatoa fursa kwa taasisi, mashirika, mabalozi, wafanyabiashara na wengine kujionea mambo mbalimbali yaliyopo katika mkoa huo.

Alisema mkoa wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya kuwekeza na kutoifanyia kazi jambo ambalo limekuwa likiwafanya wasiendelee kiuchumi.

“Tunashukuru kuwa katika awamu ya nne, tumefanikiwa kuboresha miundombinu ikiwemo barabara ya kiwango cha lami, zahanati na kiwanja cha ndege.

“Kwa upande wa kiwanja cha ndege kinaendelea kujengwa na sasa kina uwezo wa kupata ndege za FOCA na pia precission air kutokana na ukubwa wake sasa,” alisema.

Alisema lengo la kuboresha miundombinu hiyo ni kuhakikisha kuwa wakazi na watu toka sehemu tofauti wanasafiri bila tatizo.

Alisema kuwa katika kongamano hilo, litasaidia wakazi wa Kigoma kupata fursa ya kuwekeza wenyewe na kuona mambo mengi yaliyofanywa na uongozi wao.

Aliwataka wadau wenye nia ya kuwekeza katika mkoa huo waweze kufika, kwani kuna vitu vingi ikiwemo madini na makaa ya mawe na misitu kwa ajili ya kivutio cha utalii.

Chanzo: Mtanzania





0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa