Home » » Chama cha waandishi wa habari Kigoma chajiunga na LAPF

Chama cha waandishi wa habari Kigoma chajiunga na LAPF

KATIKA kukabiliana na hali ngumu kichumi Klabu ya waandishi wa habari mkoani Kigoma KGPC imejiunga na mfuko wa hifadhi ya Jamii wa LAPF ili kuwawezesha wanachama wake kujitegemea badala ya kuvitegemea vyombo vya habari ambavyo hata hivyo huwalipa maslahi duni.

Hatua hiyo inatajwa kuwa mkombozi kwa waandishi hao ambao wamekuwa tegemezi kwa muda mrefu licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi lakini pindi wanapopata matatizo ya kifamilia hukosa mahali pa kukimbilia.

Umoja wa vilabu vya habari nchini UTPC ukiwa ndio nguzo pekee ya kuwalea wanahabari hususani wanaoishi mikoani umeshiriki kwa karibu katika kuviunganisha vilabu vya habari hapa nchini na sekta mbalimbali za kifedha ili kuhakikisha mwanataaluma ya habari anaondokana na umasikini wa kipato.

Makamu wa Rais wa UTPC Bi. Jane Mihanji amesema umoja huo umekuwa ukitafuta njia mbadala ambazo zitasaidia kuwapunguzia wanahabari ukali wa maisha ambapo sasa imekuja na mbinu mpya ya kuanzisha chama cha kutetea maslahi ya waandishi.

Mwenyekiti wa KGPC Deo Nsonkolo amesema ni Klabu ya kwanza nchini kujiunga na mfuko huo, KGPC imedhamiria kuwakomboa wanachama wake kutoka kwenye lindi la umasikini ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya waandishi wa habari mkoani humu hawana ajira za kudumu kutoka kwenye vyombo wanavyofanyia kazi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa