WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kutoa fedha za kununua mizinga kati ya
100 na 200 kwa ajili ya wanakijiji wa Biturana, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma
ambao wanajihusisha na uhifadhi wa misitu pamoja na ufugaji nyuki.
Ametoa ahadi hiyo jana mchana (Alhamisi, Oktoba 3, 2013) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi wa kijiji hicho mara baada ya kukagua eneo la hifadhi ya
Biturana pamoja na baadhi ya mizinga iliyomo kwenye hifadhi hiyo.
Alisema kwa vile mizinga hiyo inatengenezwa kwenye wilaya yao kwa thamani
ya sh. 50,000 kwa kila mzinga, atawatafutia fedha za kutosha mizinga 100 -200
kulingana na mahitaji yao ambazo ni kati ya sh. milioni 5/- na sh. milioni
10/-.
Waziri Mkuu aliwashauri waanze taratibu kuachana na mizinga ya asili na
badala yake watumie mizinga ya viunzi na baada ya muda wakishaizoea itabidi
wahamie kwenye mizinga ya biashara.
“Mizinga ya viunzi ina kasoro moja kubwa kwani humfanya mfugaji alazimike
kukata sega zima, wakati hii ya kibiashara inakupa fursa ya kutoa sega
ukafyonza asali na kurudisha tena sega hilo kwenye mzinga ili nyuki waanze tena
kutengeneza asali nyingine,” alisema.
“Lakini kwa sasa hamuwezi kuanza na mizinga ya kibiashara moja kwa moja, ni
lazima kuitoa polepole huku wanakijiji wakijifunza jinsi ya kutumia hii mizinga
ya kisasa ambayo ni ya viunzi,” alisema wakati akitoa maelekezo kwa Afisa Nyuki
wa wilaya hiyo, Bw. Seif Salum Seif.
Akisoma taarifa ya mradi wao mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa Kikundi cha
Wafuga Nyuki cha Biturana, Bw. Christopher Ibrahim alisema kikundi chao ambacho
kilianzoshwa mwaka 2011, kina wafugaji 52 ambao wana mizinga 4,554 ambao kati
yao 44 ni wananume na wanane ni wanawake.
“Eneo la hifadhi ya Biturana lina ukubwa wa hekta 407.5 na kati ya mizinga
4,554, mizinga 4,457 ni ya asili na mizinga 97 ni ya kisasa.” Alisema kwenye
mizinga ya asili, mizinga zaidi ya 4,000 ina nyuki wakati ile 97 ya kisasa yote
ina nyuki ndani yake.
Kuhusu uzalishaji, Bw. Ibrahim alisema katika msimu wa mwaka 2012/2013,
wanakikundi walivuna kilo 3,550 za asali zenya thamani ya sh. milioni 5.08/- na
nta kilo 55 zenye thamani ya sh. 275,000/-.
Naye Afisa Nyuki wa Afisa Nyuki wa wilaya hiyo, Bw. Seif alimweleza Waziri
Mkuu juu ya mradi wa kuzalisha malkia wa nyuki ambao unatarajia kuanza hivi
karibuni na kwamba wameandaa mizinga 15 ambayo itatumika kwa kuzalisha malkia
kijijini hapo.
“Shirika la Maendeleo la Ubelgiji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya
ya Kibondo wameanza mpango wa kuendeleza eneo hili la hifadhi ya Biturane na
kuamua kujenga kituo cha mafunzo cha kuzalishia malkia kwa gharama ya sh.
milioni 4/-,” aliongeza.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Kigoma,
aliwahakikishia wanakijiji hao kwamba Tanzania inaweza kuwa mwamba wa
uzalishaji asali duniani na kuipiku Ethiopia ambayo hivi inaongoza kwa
kuzalisha tani 40,000 za asali kwa mwaka.
“Tukijipanga vizuri tunaweza kuwa mwamba wa uzalishaji asali duniani kwa
sababu uwezo tunao wa kuzalisha tani 100,000 kwa mwaka; misitu tunayo na mito
tunayo mingi. Wenzetu wale wana jangwa katika sehemu kubwa ya nchi yao lakini
waliiona hii fursa ya ufugaji nyuki wakaamua kuichangamkia,” aliongeza.
Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na
mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia, Naibu
Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw.
Lazaro Nyalandu pamoja na Naibu Waziri Nishati na Madini, Bw. George
Simbachawene.
0 comments:
Post a Comment