Na Adili Mhina, Kigoma
Wizara ya Fedha na Mipango -Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji inaendesha mafunzo ya maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa kigoma.
Akifungua
mafunzo hayo yanayoendelea mjini kigoma na kuwashirikisha Makatibu
Tawala, Wakurugenzi na wataalam wa sera na mipango kutoka Halmashauri
zote za Mkoa wa kigoma, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi
Florence Mwanri alieleza kuwa Serikali ya Ubelgiji ambayo ndio
iliyofadhili mafunzo hayo kuwa imefanya jitihada kubwa katika kufadhili
miradi mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma.
“Tunaishukuru sana Serikali
ya Ubelgiji kwani kwa kipindi kirefu imekuwa ikifanya kazi kubwa katika
kufadhili miradi ya maendeleo hususan kwenye sekta za kilimo na maji
ambapo kwa kiwango kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya wananchi wa
mkoa huu,” alieleza Bibi Mwanri.
Alisisitiza
kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia miradi iliyotekelezwa na
inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Ubelgiji katika Mkoa wa Kigoma
zipo changamoto kadhaa ambazo zimeonekana kupunguza ufanisi wa miradi
husika.
Miongoni mwa changamoto hizo ni; rushwa,
kiwango kisichoridhisha cha uratibu wa utekelezaji wa miradi,
uwakilishi duni katika kamati za utekelezaji wa miradi na ugumu wa
kupata taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Changamoto
nyingine ni pamoja na miundombinu mibovu hususan barabara na umeme
ambayo inachangia kutokuvutia wataalam kuishi katika mkoa wa Kigoma, na uhaba wa utaalam katika maandalizi, kutekeleza na kusimamia kwa ufanisi fedha zinazotumika kugharamia miradi ya maendeleo.
Mwanri aliongeza kuwa baada ya kubaini changamoto hizo, Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji iliona
umuhimu wa kutoa mafunzo ili kuongeza uelewa wa wataalam katika
kuainisha, kuchagua, kuchambua, kutafuta njia sahihi za ugharamiaji,
kusimamia utekelezaji, na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya
maendeleo.
Nae
Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Paul Sangawe alifafanua kuwa katika
kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21)
uwekezaji wa Umma umeongezeka ambapo kwa sasa Serikali inatumia
Shilingi za kitanzania trilioni 11.8 kila mwaka, na katika kipindi cha
miaka mitano ijayo shilingi Trilioni 59 zinatazamiwa kutumika kugharamia miradi ya maendeleo.
“Ni
muhimu kuelewa kuwa ugunduzi wa gesi, madini, nk kunaendana na ongezeko
la mapato kwa Serikali huku matumizi katika eneo la miradi ya maendeleo
nayo yakiongezeka. Hivyo, ni vyema kijiandaa mapema ili kuhakikisha
kuwa fedha zitakazopatikana zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo
tarajiwa,” alieleza Sangawe.
Kwa
mujibu wa Sangawe, matarajio katika mafunzo hayo ni pamoja na; kupata
maoni kutoka kwa washiriki kwa ajili ya maandalizi ya programu ya
ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali ya Tanzania na Ubelgiji
(2017- 2021), kuongezeka kwa ufanisi wa utekelezaji, ufuatiliaji na
tathmini ya miradi ya maendeleo na kuhakikisha kuwa maandiko yote ya
miradi ya maendeleo yanazingatia Mwongozo wa Usimamizi na Uwekezaji wa
Umma.
Sangawe
ambaye pia anasimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya
Uchumi Tume ya Mipango amewahakikishia washiriki wa mafunzo hayo kuwa
washirika wa maendeleo wanaunga mkono jitihada za Serikali katika
kuimarisha uchumi na hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili
kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa
ya kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.
0 comments:
Post a Comment