Watendaji Wanaotafuna Fedha za Miradi ya Wafadhili Mkoani Kigoma kukiona
Na Adili Mhina, Kigoma.
Serikali
imewaonya watumishi wasio waaminifu katika kusimamia na kuratibu miradi
inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa maendeleo kuepukana na vitendo
vya rushwa na ubadhirifu kwani Serikali ya Awamu ya Tano haina huruma
wala msamaha kwa watu wa aina hiyo.
Onyo
hilo limetolewa mwishoni mwa juma na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa
Kigoma Bw. Daniel Machura wakati akifunga mafunzo ya maandalizi ya
miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa
mkoa wa Kigoma yaliyofanyika mjini hapa na kuendeshwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango kwa ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji.
Mafunzo
hayo yalishirikisha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Makatibu tawala wa wilaya, Wakuu wa Idara za Mipango, Wachumi, Maafisa
Mipango na Watakwimu ambao wana majukumu ya usimamizi na uratibu wa
miradi katika sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma na Halmashauri zake zote.
Machura
alieleza kuwa Serikali ya sasa haina nafasi ya kuwalea watendaji ambao
wanaweka maslahi yao mbele badala ya kuangalia wananchi katika
kutekeleza miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo kitu
kinachopelekea miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango bila kuzingatia
thamani ya fedha.
Alieleza
kuwa baadhi ya watumishi walifikia hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba
fedha za ufadhili wa miradi ya maendeleo ya wananchi lakini fedha hizo zikipatikana walikuwa wanagawana na kuzitumia katika shughuli zao binafsi badala ya kuzingatia malengo ya fedha hizo.
“Tulifika
pabaya sana, watu walikuwa wanaandika proposal (andiko) kwa wafadhili
ili wapate fedha za kutekeleza miradi ya wananchi lakini cha ajabu
unakuta fedha zikipatikana wanagawana bila aibu kwa kuwa zimetoka nje,
katika serikali ya sasa watu wa aina hiyo hawana nafasi kwenye utumishi
wa umma,” alieleza Bw. Machura.
Alisisitiza kuwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa hawana budi kuzingatia mafunzo waliyopata kwa ajili ya kuongeza ufanisi
wa kusimamia miradi na kuleta maendeleo katika maeneo yao ya utawala
ili wafadhili waendelee kuamini kuwa fedha zote wanazotoa zinatekeleza
miradi iliyokusudiwa.
“Tukifanya
hivyo Serikali ya Ubelgiji pamoja na wadau wengine wa maendeleo
watakuwa tayari kuongeza michango yao katika kuusaidia mkoa wetu
kujikomboa kutoka katika umaskini hususan kwa kuendelea kufadhili miradi
mbalimbali ya maendeleo”, alisistiza.
Kwa
upande wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji
anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi
Tume ya Mipango, Bw. Paul Sangawe alibainisha kuwa kuna baadhi ya
watendaji ambao hawatoi taarifa za matumizi ya fedha za miradi ya
ufadhili kwa wakati, kitu ambacho kinarudisha nyuma jitihada za
washirika wa maendeleo katika kufadhili miradi.
Kutokana
na hali hiyo, Sangawe alishauri uongozi wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma
kujiwekea utaratibu wa kukaa na halmashauri zake mara kwa mara ili
kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa
maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na malengo
husika.
Aidha,
Sangawe alisisitiza kuwa ni lazima mamlaka zinazohusika katika kufanya
makubaliano ya mikataba na wafadhili kuwa makini na kuzingatia kuwa
miradi inayotaka kufadhiliwa ni ile yenye tija kwa wananchi na ambayo
inaharakisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuipeleka
Tanzania katika uchumi wa kati.
“Tusisite
kukataa miradi ambayo haina tija kwa wananchi wetu, hata kama fedha ni
zao lakini lazima ufadhili wao uendane na vipaumbele tulivyojiwekea kama
Taifa. Tusipo zingatia hilo tutajikuta tunatekeleza miradi isiyo na
faida kwa wananchi na kupelekea Serikali kupata hasara,” alisisitiza
Sangawe.
0 comments:
Post a Comment