Kila mwaka, tarehe 20 Juni, Mataifa yote
ulimwenguni huadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani (World Refugee Day). Awali
siku hiyo ilikuwa inaadhimishwa Barani Afrika peke yake ikiitwa Siku ya
Wakimbizi Barani Afrika na kuanzia mwaka 2001 Maadhimisho hayo yalianza kufanyika
Duniani kote baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuelekeza hivyo
katika kuadhimisha miaka 50 ya Sheria ya Kimataifa ya Wakimbizi.
Lengo la maadhimisho haya ya kila mwaka
ni kuhamasisha Ulimwengu kutambua uwepo wa mamilioni ya wakimbizi na watu
wengine wanaohama kutoka kwenye maeneo yao kwenda maeneo mengine ndani ya nchi
zao (internally displaced persons) kuogopa vita, migogoro na mateso.
Maadhimisho haya huwahusisha viongozi wa
serikali, watumishi wa mashirika ya misaada, watu mashuhuri na wakimbizi
wenyewe. Maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu ambayo kutoa msisitizo wa
jambo ambalo hupewa msukumo katika matamko ya mwaka husika ambapo Kauli mbiu ya
mwaka huu ni ‘Tuko Pamoja na Wakimbizi’ ikiwa na lengo la kukumbusha jukumu la kila
mmoja la kuwasaidia wakimbizi na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ambayo
yamesababisha wao kujikuta katika hali hiyo.
Kama inavyofahamika Tanzania imekuwa na
historia ndefu ya kuhifadhi wakimbizi toka nchi mbalimbali za Afrika na
kwingineko. Kwa vipindi mbalimbali wamekuwepo
wakimbizi tofauti tofauti kama vile wakati
wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za Kusini ya Afrika ambapo kulikuwa na wakimbizi
toka Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe ambao walirudi katika
nchi zao za asili baada ya ukombozi kupatikana katika nchi hizo.
Aidha, nchi yetu inaendelea kuhifadhi
wakimbizi toka nchi za jirani zinazokumbwa na migogoro ya kisiasa na kivita
hususani zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
Pembe ya Afrika kama Somalia na wachache toka nchi mbalimbali.
Maazimio ya mwaka huu, ya Siku ya Wakimbizi
Duniani yanaikuta nchi yetu ikiwa inahifadhi wakimbizi wapatao 345,000, wengi wao wakiwa wanatoka
katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambao wanahifadhiwa
katika kambi zilizoko Mkoa wa Kigoma za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli na wengine
wachache waliosalia baada ya wenzao wengi kupata uraia ambao wapo Katavi na
Tabora.
Kwa kuzingatia uwepo wa wakimbizi hao, maadhimisho
ya mwaka huu yatafanyika Dar es Salaam ambapo yatahusisha Wakimbizi wenyewe, Mashirika
ya Umoja wa Mataifa, Viongozi wa Serikali, Asasi zisizo za Kiraia, watumishi wa
Mashirika ya Misaada, na Wasanii maarufu, vyombo vya habari, wananchi na kwenye
maeneo yanayohifadhi wakimbizi katika Mikoa iliyotajwa.
Serikali yetu itapenda kutumia maadhimisho
ya mwaka huu kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa, wakimbizi wenyewe pamoja na
wadau mbalimbali kuwa itaendelea kuchukua hatua muhimu za kuboresha
huduma kwao katika sekta za elimu, afya, makazi na kuihuisha Sera ya Wakimbizi
ili ieandane na changamoto za wakati huu.
Kwa upande wa elimu, Serikali inatambua tatizo
la upungufu wa madarasa katika kambi za wakimbizi linalotokana na upungufu wa
fedha zinazotolewa na Wahisani kufadhili mradi mzima wa kuhifadhi maelfu ya
wakimbizi toka nchi za jirani na kwingineko. Pamoja na hayo, nchi yetu kwa
kushirikiana na UNHCR na wadau wengine itafanya jitihada za kujenga madarasa na
miundo mingine muhimu kuhakikisha kuwa watoto wote wa wakimbizi wanapata elimu
bora kuwawezesha kupata taaluma na ujuzi
utakaowanufaisha wao wenyewe na jamii zao wakiwa kwenye kambi na wakati
watakaporejea kwenye nchi zao za asili .
Vile vile Serikali,
kupitia taasisi yake ya RITA, inakusudia kutoa vyeti vya kuzaliwa,
kwa watoto wa wakimbizi ambao wanazaliwa hapa nchini, katika kambi za wakimbizi,
ili kuwafanya watoto hao kuwa na hati
zinazotambulika kisheria na zenye kubainisha waziwazi uraia wao wa asili. Ni
vema ikafahamika kuwa hati hizo ni muhimu hata baada ya maisha ya ukimbizi.
Uamuzi wa kuwapatia hati unafuatia
makubaliano baina ya serikali na UNHCR
yanayowezesha Shirika hilo kusaidia
nyenzo muhimu zinazohitajika katika zoezi
hilo.
Ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa
wakimbizi wanapata hati zote muhimu zinazohitajika kama cheti cha kuzaliwa,
kitambulisho n.k kwa mujibu ya Mikataba ya Kimataifa mbayo nchi imeiridhia. Ni matarajio ya Serikali kuwa vyeti
vya kuzaliwa vitaanza kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu na utakuwa ni
utaratibu wa kudumu.
Eneo jingine ambalo litapewa kipaumbele kwa
lengo la kuboresha huduma kwa wakimbizi ni mradi wa kuhuishwa Sera ya Wakimbizi
na Sheria pamoja na mambo mengine, Sera mpya
na Sheria zitakazotungwa inakusudia kupanua wigo wa wakimbizi wenye ujuzi na
sifa za kupata ajira kama wataalamu katika sekta mbalimbali na pia kupata fursa
za kujiari wenyewe nje ya kambi.
Wakati dunia inaadhimisha siku ya Wakimbizi
Duniani, ni vema pia tukaikumbusha Jumuia ya Kimataifa kuhusu wajibu wao
kuongeza ufadhili kuzisaidia nchi changa, kama Tanzania, kutekeleza jukumu la
kuhifadhi wakimbizi. Misaada wanayotoa inasaidia
katika kupatikana kwa bidhaa mbalimbali
ambazo zitatumiwa na wakimbizi na huduma nyingine wanazohitaji. Ni vema ikaeleweka pia kuwa Jumuia ya
Kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia jamii ambazo zinaathirika na uwepo wa
wakimbizi wengi kama Kagera, Kigoma,
Katavi na Kigoma.
Imetolewa na
Balozi Hassan Simba Yahya
Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
20 Juni, 2017
0 comments:
Post a Comment