ONSPOT MAGAZINE

ONSPOT MAGAZINE

WATAKA NHIF IGHARAMIE NAULI ZA WAGONJWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

BAADHI ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wametaka kuongezwa kwa huduma za malipo ya nauli na posho kwa wanachama wanaokwenda kwenye matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao, sambamba na kugharamia upimaji wa vinasaba (DNA).
Walisema hayo walipozungumza wakati wa kikao cha pamoja baina ya wanachama wa mfuko huo katika kijiji cha Mwamgongo, Kigoma Vijijini mkoani hapa na viongozi wa mkoa wa mfuko huo.
Walisema kuwa ni vizuri wanachama wanaokwenda kupata matibabu ya rufaa, wagharamiwe nauli na posho na mfuko huo.
Nassib Ally, mtumishi katika Kituo cha Afya cha Mwamgongo, alisema licha ya sasa malipo ya nauli na posho za safari kulipwa na mwajiri, lakini wakati mwingine malipo hayo hayalipwi kwa wakati.
Alisema hali hiyo huwafanya wanachama kuhangaika kufuatilia matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao vya kazi.
Mussa Boniface, mwalimu wa Shule ya Msingi Mwamgongo, alitaka mfuko kugharamia huduma za upimaji wa DNA na kugharamia huduma za matibabu ya nje ya nchi kwa wanachama wake.
Akizungumzia maombi hayo, Meneja wa NHIF mkoa wa Kigoma, Elius Odhiambo alisema kwa sasa mfuko haugharamii malipo ya posho na nauli kwa wanachama wake, wanaokwenda rufaa nje ya vituo vya kazi. Alieleza kwamba suala hilo litabaki kuwa juu ya mwajiri.
Odhiambo alisema kitendo cha kugharamia posho na nauli kwa wanachama, itawalazimu wanachama hao kuchangia zaidi.
Alieleza kwamba suala hilo linahitaji mjadala mrefu ambao utaridhiwa na wanachama wote kuweza kutekeleza hilo.
Meneja huyo pia alisema suala la maombi ya mfuko kugharamia matibabu ya nje ya nchi, litabaki chini ya wizara ya afya huku upimaji wa vinasaba ukiendelea kuwa gharama za mtu binafsi.
Chanzo;Habari leo

HIZI NDIZO SIFA ZA MWALIMU BORA- 2

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Katika makala iliyopita tuliangalia baadhi ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mwalimu. Katika makala haya tutaendelea na sifa nyingine.
Moja kati ya sifa kubwa ambayo mwalimu anatakiwa kuwa nayo ni ushirikiano kati yake na walimu wenzake, wanafunzi na wazazi kwa jumla.
Ushirikiano na walimu wenzake utamwezesha kufanya kazi yake vizuri, lakini pia kuboresha upeo wa fikra na taaluma kwa jumla.
Ama kwa upande wa wanafunzi, ushirikiano utaondoa kizuizi kati yake na wanafunzi na utawaweka huru wanafunzi kuweza kumhusisha pale wanapokuwa na matatizo mbalimbali.
Wazazi pia wanatakiwa washirikishwe katika kujua maendeleo ya watoto wao shuleni. Katika kufanikisha hili mwalimu ana nafasi kubwa.
Pia, mwalimu anatakiwa awe muumini mkubwa wa nidhamu. Mwalimu anatakiwa asifumbie macho vitendo vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi na avikemee bila kupepesa macho.
Hivi sasa kuna changamoto kubwa katika kudhibiti nidhamu za wanafunzi ukizingatia kuwa adhabu ya viboko imekatazwa shuleni. Lakini pamoja na kukatazwa huku kwa adhabu ya viboko bado mwalimu ana wajibu wa kutumia mbinu mbadala katika kudhibiti nidhamu za wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa nidhamu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya taaluma. Katika kudhibiti nidhamu mwalimu anatakiwa yeye mwenyewe ajiheshimu. Haipendezi kumwona mwalimu akiwa amevaa mavazi yasiyo na stara yanayoonesha utupu kwa wanawake au kuvaa mlegezo kwa wanaume.
Pia, kujichora katika mwili au kuvuta bangi na dawa za kulevya. Huwezi kudhibiti nidhamu za wanafunzi kama wewe mwenyewe hujiheshimu.
Mwalimu hatakiwi kuwa mwoga na kuogopa kukosolewa katika masuala yanayohusu taaluma. Uthubutu ni katika sifa zilizotukuka za mwalimu. Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa ziada wa kuchagiza maendeleo ya wanafunzi na kutatua matatizo mbalimbali yanayohusu taaluma na wanafunzi kwa jumla.
Anatakiwa awape moyo wanafunzi wake nao wajifunze kutoka kwake ili waweze kufanikiwa kitaaluma na kimaisha.
Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa kuwahusisha wanafunzi wake ili waweze kufuatilia masomo darasani. Wanafunzi wana maarifa mbalimbali ambayo mwalimu pia anaweza kunufaika nayo akitaka.
Usiwachukulie wanafunzi wako kama watu wasio na kitu kichwani na usitawale darasa kana kwamba wewe ndiye mjuzi wa kila jambo. Washirikishe na wajengee wanafunzi wako uwezo wa kujiamini na kutenda na huu ndiyo msingi mkubwa katika maendeleo ya taaluma.
Kuwa na moyo wa huruma na kusamehe ni sifa iliyotukuka ya mwalimu. Mwalimu si mtu wa kuendekeza malumbano yasiyo na tija kwa wanafunzi wake na walimu wengine. Mazingira ya amani na utulivu shuleni ni muhimu kwa maendeleo ya taaluma.
Sifa ni nyingi, lakini ningependa tutosheke na hizi chache ambazo zinaweza kuwakumbusha walimu thamani yao na umuhimu wao katika kuendeleza taaluma.
Ni vizuri nikiwakumbusha walimu kuwa ualimu ni mojawapo ya kazi tukufu kabisa katika historia ya mwanadamu na hakuna jamii yoyote iliyofanikiwa bila ya kuwa na walimu bora.
Hivyo, pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, wajithamini na watambue kuwa wana mchango mkubwa katika kuikomboa jamii kutokana na adui ujinga na hatimaye kuiletea maendeleo.
Rajabu Kipango ni mwalimu na mtaalamu wa rasilimali watu.
Chanzo;Mwananchi

KIGOMA WATAKIWA KUCHANGAMKIA MAONYESHO YA WAJASIRIAMALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WANANCHI wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kutumia fursa waliyoipata ya maonyesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati Kanda ya Kati kwa kujitangaza kibiashara na kujifunza kutoka kwa wenzao ndani na nje ya nchi.
Akizungumza mjini hapa jana katika kikao kilichohusisha viongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (Sido), na Waandishi wa Habari, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu Issa Machibya, alisema maonyesho hayo yatafanyika Community Centre kuanzia Agosti 27 hadi Septemba Mosi na kujumuisha mikoa mbalimbali ya hapa nchini pamoja na nchi za Kenya, Uganda, DRC na Burundi.
Alisema kuwa maonyesho hayo hufanyika kwa mwaka mara moja nchini na mwaka huu Mkoa wa Kigoma umepata nafasi hiyo, hivyo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujitangaza na kujifunza, kwani itachukua miaka mingi kujirudia tena.
Machibya, alisema kutakuwepo na waonyeshaji 302 ambao wamethibitisha kushiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi, pia Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zitakuwepo kama TBS, NMB, Tanapa, Benki ya Posta na nyinginezo.
Aliongeza kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo wa hapa nchini, kupata fursa ya kukuza soko la bidhaa zao hususan mikoa ya kanda ya kati na nje ya nchi, pamoja na kujifunza kutoka kwa wenzao wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Machibya aliongeza kuwa kauli mbiu ya maonyesho hayo ni ‘Buni, Boresha, Fanya Biashara Kupitia Sido’.
Naye Meneja wa Sido mkoani hapa, Macdonard Maganga, alisema pamoja na wajasiriamali kuja katika maonyesho hayo kwa lengo la kuonyesha bidhaa zao, lakini pia ni fursa nzuri kwa wananchi wa hapa nchini kujitangaza, pia kuchukua ujuzi kutoka kwa wageni.
Chanzo;Tanzania Daima

“UNYAMA KWA ALBINO KUATHIRI AMANI YA NCHI”

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeonya kuwa unyama unaofanywa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), yatasababisha Tanzania kufutika kwenye ramani ya visiwa vya amani duniani.
Taarifa ya Kamishna wa Tume hiyo, Ali Hassan Rajab, imeeleza hayo na kuitaka Serikali na vyombo vyake vya dola, kuchunguza kwa kina waganga wa jadi, kutokana na madai kuwa ndio wanaochochea vitendo hivyo.
Rajab katika taarifa hiyo, alitoa mwito kwa Serikali na vyombo vya dola, kufanya uchunguzi wa kina kubaini wanaochochea, kufadhili na kutekeleza vitendo hivyo vya kinyama na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
“Kutokana na kuibuka tena kwa vitendo hivyo, ni dhahiri watu wenye ulemavu wa ngozi hivi sasa wanaishi kwa hofu na wanashindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru, ikiwemo kujipatia riziki zao.
"Wanaporwa haki nyingine nyingi za binadamu kama haki ya kuishi, elimu na uhuru wa mtu kwenda atakako," ilieleza taarifa hiyo na kuitaka Serikali kutumia matokeo ya tafiti zilizokwishafanywa na wadau mbalimbali kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Chanzo;Habari Leo

BOMU LARUSHWA NDANI YA BASI KIGOMA, WATATU WAUAWA, SITA WAJERUHIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Watu watatu wamekufa akiwepo mtoto mchanga na wengine sita kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria (Hiace) kurushiwa bomu na watu wasiojulikana huko Kasesema, Kigoma alfajiri ya leo.
AKithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Buhigwe (OCD), Samwel Utonga alisema basi hilo lilikuwa likotokea Kilelema kwenda Kasulu Mjini ambapo watu hao walilirushia kitu kinachoaminika kuwa ni bomu.
Taarifa kutoka Hospitali ya Muyama zinazema majeruhi hao wamehamishwa toka hospitalini hapo na kupelekwa Hospitali ya Kasulu  baada ya hali zao kuwa mbaya
chanzo;Mwananchi

ZITTO KUPEWA ULINZI NA ACT

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

CHAMA cha Alliance Transparency For Change (ACT) Mkoa wa Kigoma, kimeahidi kumlinda na kumtetea Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), kutokana na changamoto zinazomkumba kupitia watu wachache wanaotaka kumwangusha kisiasa.

Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya chama hicho, Bw. Jaffar Kasisiko, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Cine Atlas, kwenye Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Alisema chama hicho hakipo tayari kuyafumbia macho matatizo yanayomkuta Bw. Kabwe na kumshauri mbunge huyo aachane na CHADEMA badala yake ajiunge na ACT ili aweze kukusanya wanachama kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata na wilaya.

Aliongeza kuwa, uongozi wa CHADEMA una hila ya kusambaza maneno kwa umma dhidi ya Bw. Kabwe ili kulinda masilahi yao binafsi badala ya kutetea haki za wanyonge.

“Kabwe asipoteze muda wa kulumbana na uongozi wa CHADEMA, huu ni wakati mwafaka kwake kufanya uamuzi makini wa kwenda kuifuta kesi dhidi ya chama chake mahakamani na kujiunga na ACT,” alisema Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Msafiri Wamalwa.

Katibu Mwenezi Wilaya ya Kigoma kutoka chama hicho, Anzoluni Kibela, alisema ACT imeandaa kadi kwa ajili ya Bw. Kabwe ambapo kuna wabunge 18 wapo tayari kujiunga na chama hicho kwenye uzinduzi rasmi ulipangwa kufanyika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Shaban Mambo, aliwasihi wananchi wamuunge mkono Bw. Kabwe atakapojiunga na chama hicho ili aboreshe hali ya usafiri wa reli ya kati kwa kuwaletea treni inayotumia umeme kwa gharama zake.

Baadhi ya wanachama wapya wa ACT akiwemo aliyekuwa Mweka Hazina wa CHADEMA Kigoma Ujiji, Bw. Hamidu Hamis na Katibu wa ACT wilayani humo, Bw. Haji Idd, walisema wamejiunga na chama hicho ili kuleta uwazi uwajibikaji

Chanzo;Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa